Available languages:
KATIBU MKUU WA UN NA OMBI LA KIMATAIFA KUSHUGHULIKIA NA KUPAMBANA NA KAULI ZA CHUKI WAKATI WA COVID-19
8 May 2020 -  COVID-19 haijali sisi ni kina nani, tunaishi wapi, tunaamini nini au kuhusu tofauti nyingine yoyote. Tunahitaji kila aina ya mshikamano kulikabili janga hili kwa pamoja. Lakini bado janga hili linaendelea kuzusha tsunami ya chuki na chuki dhidi ya wageni, ubebeshaji lawama na vitisho.

Mtazamo wa kupinga wageni umeenea mtandaoni na mabarabarani. Nadharia za kupinga Uyahudi zimesambaa na mashambulizi yanayoambatana na COVID-19 dhidi ya Uislam yamefanyika. Wahamiaji na wakimbizi wametajwa kama chanzo cha virusi na kisha kunyimwa huduma za matibabu.

Pamoja na wazee kuwa miongoni mwa walio hatarini zaidi dharau zimeibuka zikionyesha kuwa na wao pia ndio wanaokumbwa zaidi. Na waandishi wa Habari, wanaodokeza ukweli, wataalam wa afya, wafanyakazi wa misaada na watetezi wa haki za binadamu wanalengwa kwa sababu tu ya kufanya kazi zao.

Tunapaswa kuchukua hatua sasa kuimarisha kinga ya jamii zetu dhidi ya virusi vya chuki. Ndio maana ninatoa ombi leo la juhudi za kila namna kukomesha kauli za chuki duniani.

Natoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuonyesha mshikamano na watu wote wa jamii zao na kujenga na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

Natoa wito kwa taasisi za elimu kuzingatia ufundishaji wa kidijitali wakati ambao mabilioni ya vijana wako mtandaoni na wakati ambao wenye itikadi kali wanatafuta kuwinda mateka na hatimaye kurubuni watu hao.

Natoa wito kwa wanahabari na hususan makampuni ya mitandao ya kijamii kufanya juhudi zaidi kulingana na sheria za kimataifa za haki za binadamu, kuondoa ubaguzi wa rangi, mila potofu na maudhui mengine mabaya.

Natoa wito kwa asasi za kiraia kuimarisha hatua za kuwafikia watu walio katika mazingira hatarishi na wadau wa kidini kutumika kama mifano ya kuheshimiana.

Namtaka kila mtu kila mahali asimame dhidi ya chuki, mtendeane utu na kutumia kila fursa kueneza wema. Mwaka jana nilizindua mkakati na mpango wa hatua wa Umoja wa Mataifa dhidi ya kauli za chuki ili kuimarisha juhudi za Umoja wa Mataifa dhidi ya jinamizi hili.

Tunapopambana na janga hili tuna wajibu wa kulinda watu, kutokomeza unyanyapaa na kuzuia machafuko.

Hebu na tuzishinde kauli za chuki na janga la COVID-19 kwa pamoja.