Available languages:
(Kiswahili) António Guterres (UN Secretary-General) Special Appeal to Religious Leaders - 11 April 2020
11 Apr 2020 -  Leo, nataka kutoa ombi maalum kwa viongozi wa imani zote za dini kuunganisha jitihada zao kusongesha amani duniani kote na kujikita katika lengo letu moja la kutokomeza COVID19.

Ninafanya hivyo katika wakati huu muhimu wa kalenda ya kidini.

Kwa wakristu, ni sikukuu ya Pasaka. Kwa wayahudi ni Pasaka ya wayahudi. Na punde, waislamu wataanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Natuma salamu zangu za dhati kwa wale wote wanaotambua nyakati hizi muhimu.

Kila mara tumetambua matukio haya kama nyakati za jamii zetu. Familia kukutana pamoja. Kukumbatiana, kushikana mikono na kukusanyika kwa ajili ya utu.

Lakini zama za sasa ni tofauti.

Sote tunahaha kukabili zama za ajabu na ulimwengu wa ndoto.

Dunia yenye mitaa iliyo kimya. Maduka yamefungwa. Sehemu kimya za ibada.

Na ulimwengu wenye hofu.

Tunahofia kuhusu wapendwa wetu ambao nao wanahofu juu yetu.

Tunasherehekea namna gani nyakati kama hizi?

Hebu tusake hamasa kutoka katika misingi ya matukio haya matakatifu kama fursa ya tafakari, kumbukizi na kuchanua upya.

Na tunapotafakari, hebu na tuwe na fikra mahsusi kwa wahudumu wa afya mashujaa walio mstari wa mbele kukabiliana na virusi vibaya – na wale wote wanaofanya kazi kusongesha majiji na miji yetu.

Hebu na tukumbuke wale walio hatarini zaidi duniani kote. Wale walioko kwenye kanda za mapigano na kambi za wakimbizi, makazi duni na wale wote walioko kwenye maeneo yasiyo na vifaa sahihi kukabiliana na virusi vya Corona.

Na hebu turejeshe upya imani yetu kwa kila mtu na kupata uthabiti kutokana na mambo mazuri yaliyopo nyakati mbaya wakati huu ambapo jamii zenye imani na tamaduni tofauti zinaungana ili kusaidiana.

Kwa pamoja tunaweza kushinda virusi hivi – kwa ushirikiano, mshikamano na imani katika utu wetu wa pamoja.