Available languages:
António Guterres (Katibu Mkuu) Ujumbe a Siku Ya Kimataifa Ya Bayoanuai 2021
21 May 2021 -  Dunia yenye afya ni muhimu sana katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Wakati huohuo Bayoanuai inapungua kwa kasi inayoleta taharuki na shinikizo zaidi ya kuilinda kila kukicha.

Tunatumia rasilmali kwa kasi kubwa kuliko zinavyozalishwa na mazingira yetu ya asili.

COVID-19 imetukumbusha zaidi kuhusu uhusiano wa karibu uliopo baina ya watu na mazingira ya asili.

Janga hili linalotukumba sasa hivi linatupa fursa ya kutathmini jinsi ya kurejea shughuli za kawaida kwa ubora zaidi.

Tunahitaji kulinda mazingira yetu ya asili, kurejesha mifumo ya ikolojia na kuishi kwa uwiano unaofaa katika uhusiano wetu na dunia.

Manufaa ni mengi.

Kwa kurejesha Bayoanuai iliyopotea, tunaweza kuboresha afya ya binadamu, kuwezesha Malengo ya Maendeleo Endelevu na kushughulikia dharura inayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Suluhu zipo zinazotuwezesha kulinda muundo halisi wa dunia yetu katika ardhi na katika bahari.

Kila mtu anajukumu analopaswa kutekeleza.

Kuchagua maisha yenye uendelevu ndiyo jibu sahihi.

Ni muhimu kila mtu kila mahali aweze kuwa na uhuru wa kuishi kwa njia ambayo ina uendelevu.

Na hivyo inamaanisha kuwa na sera nzuri zaidi zinazohamasisha uwajibikaji wa serikali, biashara na mtu binafsi. Sote tunapaswa kuwa sehemu ya mchakato unaoleta mabadiliko.

Mwaka huu serikali zitakutana Kunming, China, na kukubaliana kuhusu mfumo wenye mtizamo mpana wa dunia kwa ajili ya bayoanuai.

Tuungane na ari yao kwa kutetea mazingira yetu ya asili.

Katika Siku hii ya Kimataifa ya Bayoanuai, sote tuwe sehemu ya suluhisho.