Available languages:
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa UN António Guterres kwa kumbukizi ya miaka 15 tangu kushambuliwa kwa ofisi za ujumbe wa UN nchini Iraq
10 Aug 2018 -  Miaka 15 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulipata pigo kubwa katika historia yetu.

Tarehe 19 Agosti mwaka 2003, shambulizi la kigaidi lililotokea katika makao yetu makuu kwenye Hoteli ya Canal mjini Baghdad, na kuua watu 22 na kuwajeruhi wengine wengi.

  Tunawakumbuka wenzetu waliopoteza maisha wakipigania amani, maendeleo na haki za binadamu.

Miongoni mwao, alikuwepo mwakilishi wetu nchini Iraq, marehemu Sergio Viera de Mello.

Nilikutana na Sergio mara nyingi na kufuatilia kwa ukaribu kazi yake nzuri nchini Timor-Leste. Nilivutiwa na jinsi alivyotilia maanani maadili ya Umoja wa Mataifa na ari yetu ya kutoa huduma.

Leo tunawaenzi wote waliofariki dunia katika zahma hiyo mbaya kabisa miaka 15 iliyopita.

Tunaenzi kujitolea kwao. Tutaendeleza kazi yao. Na daima tutawakumbuka tukijitahidi kutatua na kuzuia migogoro ya silaha na kujenga dunia yenye ustawi na amani kwa wote.

 Asante