Available languages:
Wito Wa Katibu Mkuu Wa Un Kuhusu Usitishaji Uhasama Duniani
23 Mar 2020 -  Dunia yetu inakabiliwa na adui wa pamoja: COVID-19.
Virusi havijali kuhusu utaifa au ukabila, kikundi au imani. Vinatushambulia wote bila huruma.
Wakati huohuo vita vya silaha vimetawala duniani kote.
Wale wasiojiweza -wanawake na watoto, watu wenye ulemavu, waliotengwa na waliotawanywa ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi.
Na ndio walio katika hatari kubwa ya kukabiliwa na athari mbaya kutokana na COVID-19.
Hebu na tusisahau kwamba nchi zilizoghubikwa na vita mifumo ya afya imesambaratika.
Wahudumu wa afya tayari ni wachache na mara nyingi wanalengwa.
Wakimbizi na watu wengine waliotawanywa na machafuko wako hatarini mara mbili.
Hasira ya virusi inaonyesha upumbavu wa vita.
Ndio maana leo hii, ninatoa wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano haraka katika pembe zote za dunia.
Ni wakati wa kuifunga migogoro ya silaha na kujikita pamoja kwenye mapambano ya kweli ya maisha yetu.
Kwa pande kinzani, nasema:
Jiengueni kutoka kwenye uhasama.
Wekeni kando kutoaminiana na chuki
Nyamazisheni silaha, komesheni mashambulizi ya makombora, malizeni mashambulizi ya anga.
Hili ni muhimu sana…
Katika kusaidia kutoa mwanya wa misaada ya kuokoa maisha.
Kufungua njia kwa ajili ya diplomasia.
Kuleta matumaini katika maeneo ya walio hatarini kwa COVID-19
Hebu tuchukue msukumo kutoka kwa umoja na mazungumzo ambayo taratibu yanaanza kuchukua sura mpya miongoni mwa pande kinzani ili kuwezesha mtazamo wa pamoja dhidi ya COVID-19. Lakini tunahitaji zaidi ya hayo.
Tumalize madhila ya vita na kupambana na ugonjwa ambao unaisambaratisha dunia yetu.
Inaanza kwa kusitisha mapigano kila mahali sasa
Hilo ndilo familia ya ubinadamu wetu inalihitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote.