Available languages:
Katibu Mkuu Wa Umoja Wa Mataifa Ujumbe Wa Video Kuhusu Wanawake Na Covid-19
9 Apr 2020 -  Janga la COVID-19 linaathiri kila mtu, kila mahali

Lakini madhara yake ni tofauti kwa makundi tofauti , na huchochea ukosefu wa usawa.

Takwimu za awali zinadokeza kuwa kiwango cha vifo vya COVID-19 kinaweza kuwa kikubwa kwa wanaume. Lakini janga hili lina madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa wanawake na wasichana.

Leo hii tunazindua ripoti inayoonesha jinsi COVID-19 inaweza kurudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana katika usawa na haki za wanawake na inapendekeza njia za kuweka uongozi wa wanawake na michango yao katika msingi wa mnepo na kujikwamua.

Takribani asilimia 60 ya wanawake duniani kote wanafanya kazi kwenye sekta ya uchumi isiyo rasmi, kwa kipato kidogo, akiba ndogo na wako hatarini kutumbukia kwenye umaskini.

Kadri masoko yanavyoporomoka na biashara kufungwa, mamilioni ya ajira zinazofanywa na wanawake zinapotea.

Na wakati huo huo kadri wanavyopoteza ajira za malipo, kazi zao za malezi wanazofanya bila malipo zinazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa wakati kutokana na shule kufungwa na ongezeko la wazee.

Mienendo ya sasa inachangamana kuliko wakati wowote ule kutwamisha haki za wanawake na kuwanyima fursa zao.

Hatua zilizopigwa zikipotea, huchukua miaka kadhaa kurejesha. Watoto wa kike wasiokuwepo shule wanaweza wasirudi tena.

Nasihi serikali ziweka masuala ya wanawake na wasichana kwenye kitovu cha harakati za kujikwamua baada ya COVID-19.

Hii inaanza na wanawake kuwa viongozi wakiwa na uwakilishi sawa kwenye mamlaka za kutoa uamuzi.

Mikakati ya kulinda na kuchochea uchumi, kuanzisha upatiaji watu fedha hadi mikopo lazima ilenge wanawake.

Mifuko ya hifadhi ya jamii lazima ipanuliwe.

Kazi za malezi zisizo na malipo lazima zitambuliwe na zithaminiwe kama mchango muhimu kwenye uchumi.

Janga hili pia limesababisha ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake.

Takribani mwanamke 1 kati ya 5 duniani kote alikumbwa na ukatili mwaka uliopita.

Idadi kubwa ya wanawake hao wamenasa majumbani wakiwa na wakatili wao, wakihaha kupata huduma ambazo sasa zimepunguzwa au zina vikwazo.

Huu ndio msingi wa ombi langu kwa serikali mapema wiki hii kuchukua hatua za haraka kulinda wanawake na kupanua wigo wa huduma hizo.

COVID-19 siyo tu changamoto ya mifumo ya afya duniani, bali pia ni jaribio la utu wetu wa pamoja.

Usawa wa jinsia na haki za wanawake ni muhimu katika kuondoka na hili jangwa pamoja, kujikwamua harua na kujenga mustakabali bora kwa kila mtu.