Available languages:
Salamu za mwaka mpya wa 2019 kutoka kwa Katibu Mkuu wa UN
29 Dec 2018 -  Wapendwa raia wenzangu wa dunia, Nawatakia heri ya mwaka mpya wenye furaha, amani na ustawi.
Mwaka mpya uliopita, nilitangaza hali ya tahadhari, na hatari nilizozitaja bado zipo. Hizi ni nyakati za wasiwasi kwa watu wengi, na dunia yetu inapitia katika majaribu mazito.
Mabadiliko ya tabianchi yanaenda kasi kuliko sisi.
Migawanyiko ya kisiasa na kijiografia inazidi kuongezeka na kufanya migogoro iwe migumu kutatulika.
Na idadi kubwa ya watu wanahama kutafuta usalama na ulinzi.
Ukosefu wa usawa unaongezeka. Na watu wanahoji dunia ambamo kwayo watu wachache wanamiliki nusu ya utajiri wa watu wote.
Ukosefu wa stahamala unaongezeka.
Uaminifu unapungua.
Lakini pia kuna sababu za matumaini.
Mazungumzo ya Yemen yametengeneza fursa ya amani.
Makubaliano yaliyotiwa saini mjini Riyadh mwezi Septemba kati ya Ethiopia na Eritrea yamepunguza msuguano wa muda mrefu na yameleta matarajio katika ukanda mzima.
Na makubaliano kati ya pande kinzani kwenye mzozo wa Sudan Kusini yamechochea fursa ya amani, na kuleta maendeleo katika miezi minne iliyopita kuliko hata miaka minne iliyotangulia.
Umoja wa Mataifa uliweza kuleta nchi pamoja huko Katowice na kuridhia mpango kazi wa utekelezaji wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.
Sasa tunahitaji kuongeza kiwango cha matarajio yetu ili kutokomeza tishio lililopo.
Ni wakati wa kutumia fursa yetu bora ya mwisho. Ni wakati wa kukomesha mabadiliko ya tabianchi yasiyodhibitika na yanayoongezeka.
Katika wiki za karibuni, Umoja wa Mataifa umeshuhudia mikataba miwili ya kihistoria kuhusu uhamiaji na wakimbizi, ambayo itasaidia kuokoa maisha na kukabiliana na fikra haribifu.
Na kila pahali, watu wanahamasishana kuhusu malengo ya maendeleo endelevu- makubaliano yetu ya kimataifa kwa ajili ya amani, haki na ustawi wa sayari iliyo bora.
Pindi ushirikiano wa kimataifa unapofanya kazi, dunia inashinda.
Mwaka 2019, Umoja wa Mataifa utaendelea kuleta watu pamoja kujenga madaraja na kuweka fursa za kusaka suluhu.
Tutaendelea na shinikizo hilo.
Na katu hatutokata tamaa.
Na tunapoanza mwaka huu mpya, hebu na tuazimie kukabiliana na vitisho, kutetea utu wa binadamu na kujenga mustakabali bora—pamoja.
Nawatakia nyote na familia zenu mwaka mpya wenye amani na ustawi.