Available languages:
KATIBU MKUU -- UJUMBE WA VIDEO JUU YA UZINDUZI WA SERA KUHUSU UTALII NA COVID-19
25 Aug 2020 -  Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zaidi kiuchumi Ulimwenguni. Inatoa ajira kwa mtu mmoja katika kila watu kumi duniani huku ikitoa riziki kwa mamia ya mamilioni zaidi. Inakuza uchumi na kuwezesha nchi kustawi. Inaruhusu watu kuendeleza utajiri wa kitamaduni na asili na kuwaunganisha watu na kuonyesha utu wetu. Kwa kweli, mtu anaweza kusema kuwa utalii wenyewe ni moja ya maajabu ya ulimwengu. Ndio maana imeleta maumivu makali kuona jinsi ambavyo utalii umeharibiwa na janga la COVID-19. Katika miezi mitano ya mwanzo wa mwaka huu, zaidi ya nusu ya watalii wanaowasili kimataifa walipungua na dola bilioni 320 katika mauzo ya nje kutokana na utalii zilipotea. Kwa jumla, ajira za moja kwa moja milioni 120 katika utalii ziko hatarini. Wengi wako kwenye sekta za uchumi zisizo rasmi au katika biashara ndogondogo, ndogo na za kati, ambazo huajiri idadi kubwa ya wanawake na vijana. Janga hili ni mshtuko mkubwa kwa uchumi ulioendelea, lakini kwa nchi zinazoendelea ni dharura, haswa kwa nchi nyingi ndogo za visiwani zinazoendelea na nchi za Afrika. Kwa wanawake, jamii za vijijini, watu asilia na watu wengine wengi waliotengwa kihistoria, utalii umekuwa chombo cha kuwaunganisha, kuwawezesha na kutengeneza kipato. Utalii pia ni nguzo muhimu kwa uhifadhi wa urithi wa asili na kitamaduni. Kupungua kwa mapato kumesababisha kuongezeka kwa ujangili na uharibifu wa makazi ya viumbe na kuzunguka maeneo yaliyotengwa, na kufungwa kwa Sehemu nyingi za Urithi wa Dunia kumeinyima jamii riziki. Ni muhimu kwamba tuijenge tena sekta ya utalii. Lakini lazima iwe katika njia iliyo salama, sawa na rafiki kwa tabianchi. Uzalishaji wa gesi ukaa itokanayo na usafirishaji unaweza kuongezeka tena ikiwa ari ya kusimama upya haitolinganishwa na malengo ya tabianchi. Kusaidia mamilioni ya watu ambao wanategemea utalii inamaanisha kujenga usafiri endelevu na wenye uwajibikaji ambao ni salama kwa jamii wenyeji, wafanyakazi na wasafiri. Ili kusaidia kusimama upya, nimeainisha maeneo matano ya kipaumbele. Kwanza, kupunguza athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na janga hili. Pili, kujenga ustahimilivu katika msururu wa thamani kwenye utalii. Tatu, kuongeza utumiaji wa teknolojia katika tasnia ya utalii. Nne, kukuza uendelevu na ukuaji imara. Na ya tano, kukuza ushirikiano ili kuwezesha utalii kusaidia zaidi Malengo ya Maendeleo Endelevu. Tuhakikishe utalii unarejea tena kwenye nafasi yake kama mtoaji wa ajira,kipato thabiti na ulinzi wa urithi wetu wa kitamaduni na asili. Asante.
Recent Video On Demand