Available languages:
Ujumbe wa Antonio Guterres kufuatia WFP kushinda tuzo ya amani ya Nobel 2020
9 Oct 2020 -  Nimefurahishwa na uamuzi wa Kamati ya Nobel kuituza tuzo ya mwaka huu ya amani ya Nobel kwa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP.
Nampongeza kwa dhati David Beasley, Mkurugenzi MTendaji wa WFP na wafanyakazi wote kwa kutambuliwa huku.
WFP ni shirika kubwa linaloongoza duniani kwa kukabiliana na ukosefu wa chakula.
Katika miaka yangu 10 ya ukamishna wa UNHCR, nilipata bahati kufanya kazi kwa ushirikiano na WFP.
Nimeshuhudia wengi wao wakifanya kazi maeneo ya ndani zaidi na hatari kwa ujasiri mkubwa na kwa ujuzi, wakihudumia watu walio hatarini zaidi duniani.
Katika dunia yenye utajiri, ni jambo lisilokubalika mamilioni ya watu wanalala njaa kila siku. Mamilioni zaidi hivi sasa wako hatarini kutumbukia kwenye njaa kutokana na janga la COVID-19.
Halikadhalika kuna kiu ya ushirikiano wa kimataifa kote duniani. WFP inakidhi hitaji hilo pia. WFP inafanya kazi bila kuangalia siasa huku mahitaji ya kibinadamu yakiwa ndio kichocheo cha kazi zake.
Shirika hili lenyewe linajiendesha kwa kutegemea michango ya hiari kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na umma.
Aina hiyo ya mshikamano ndio jambo hasa linalohitajika kushugulikia siyo tu janga, bali pia changamoto zingine za sasa. Tunafahamu kuwa vitisho kama vile mabadiliko ya tabianchi vinaweza kusababisha janga la njaa kuwa kubwa zaidi. Tunafahamu kuwa kutokomeza njaa ni muhimu kwa ajili ya amani.
Dunia yenye njaa si dunia yenye amani.
Napongeza wanawake na wanaume wa WFP, na bila shaka timu nzima ya Umoja wa Mataifa kwa juhudi zao za kusongesha amani na maadili ya Umoja wa Mataifa kila uchao.
Recent Video On Demand