Available languages:
Salamu za mwaka mpya wa 2020 kutoka kwa Katibu Mkuu wa UN
29 Dec 2019 -  Kutoka hapa Umoja wa Mataifa naungana nanyi kuukaribisha mwaka mpya.
Tunaingia mwaka 2020 tukiwa na hali ya sintofahamu na ukosefu wa usalama pande zote duniani.
Kuendelea kwa pengo la usawa na ongezeko la chuki.
Ulimwengu wenye migogoro na sayari yenye ongezeko la joto.
Mabadiliko ya tabianchi sio tu tatizo la muda mrefu bali pia ni hatari iliyo bayana na inayoendelea.
Hatuwezi kumudu kuwa kizazi kilichozembea wakati sayari ikiteketea.
Lakini kuna matumaini.
Mwaka huu, ujumbe wa Mwaka Mpya ni chanzo kikubwa zaidi cha tumaini hilo: vijana wa ulimwengu huu.
Kuanzia hatua za mabadiliko ya tabianchi hadi usawa wa kijinsia hadi haki ya kijamii na haki za binadamu, kizazi chako kiko mstari wa mbele na kwenye vichwa vya habari.
Nimetiwa moyo na shauku na azma yako.
Uko sahihi kudai jukumu katika kuunda mustakabali wetu.
Nipo pamoja nawe.
Umoja wa Mataifa unasimama na wewe - na ni wako.
Mwaka 2020 ni maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa.
Tunazindua muongo wa hatua kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, muongozo wetu kwa utandawazi wenye usawa.
Mwaka huu, dunia inahitaji vijana kuendelea kupaza sauti. Kuendelea kufikiria mambo makubwa. Kuendelea kusukuma mipaka.
Na kuendelea kutoa shinikizo.
Nakutakia amani na furaha kwa mwaka 2020.
Asante.