Available languages:
António Guterres (Katibu Mkuu wa UN) kuhusu ukatili wa kijinsia na COVID-19
5 Apr 2020 -  Tamko la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhusu Ukatili kwa misingi ya Kijinsia na COVID-19.
Janga la COVID-19 linasababisha machungu ya kibinadamu yasiyoelezeka na uharibifu wa kiuchumi duniani kote.
Hivi karibuni nilitoa wito wa kusitisha mapigano kote duniani ili tujikite katika kukabiliana na janga hili.
Nilitoa wito kumaliza ghasia kila mahali, sasa. Lakini ghasia si katika uwanja wa vita pekee.
Kwa wanawake wengi na wasichana, vitisho vimeshamiri pale ambapo panatakiwa pawe salama zaidi kwao. Majumbani mwao.
Na hivyo natoa wito mpya leo hii kwa amani iwepo majumbani na katika nyumba, duniani kote.
Tunafahamu kuwa marufuku ya kusalia majumbanj na karantini ni muhimu katika kuzuia maambukizi ya COVID-19. Lakini pia yanaweza kufanha wanawake kuwa kwenye mtego na wapenzi wao makatili.
Katika wiki moja iliyopita kadri mashinikizo ya kiuchumi na kijamii yanavyoongezeka duniani, vivyo hivyo ongezeko la vitendo vya ukatili majumbani.
Katika baadhi ya nchi, idadi ya wanawake wanaopiga simu kusaka huduma za usaidizi imeongezeka maradufu.
Wakati huo huo, wahudumu wa afya na polisi wamezidiwa uwezo na ni wachache.
Vikundi vya kijamii navyo vimedhoofika au havina fedha. Vituo vya kuhifadhi manusura wa Ukatili majumbani vimefungwa, vingine vimejaa.
Natoa wito kwa serikali zifanye huduma za kinga ya ukatili dhidi ya wanawake kuwa sehemu muhimu ya mikakati yao ya kitaifa ya kukabiliana na COVID-19.
Hii ina maana kuongeza uwekezaji katika huduma za kusaka usaidizi kwa njia ya mtandao pia kuimarisha mashirika ya kiraia.
Halikadhalika mifumo ya mahakama iendelee kushtaki wahalifu wa ukatili majumbani.
Ziandae mifumo ya kutoa tahadhari kwenye maduka ya dawa na vyakula.
Zitangaze kuwa makazi ya manusura ni huduma muhimu.
Na ziweke njia salama kwa wanawake kusaka msaada bila ufahamu wa waliowatendea uovu.
Haki za wanawake na uhuru ni muhimu kujenga jamii thabiti na zenye mnepo.
Pamoja tunapopambana ma COVID-19, tunaweza na tunapaswa kuzuia ukatili popote, kuanzia majumbani hadi uwanja wa vita.