Available languages:
Katibu Mkuu Ujumbe Wa Video Wa Mwaka Mpya 2021
28 Dec 2020 -  Wapendwa marafiki,
Mwaka wa 2020 umekuwa mwaka wa majaribu, misiba na majonzi.
COVID-19 imebadili maisha yetu na kuutumbukiza ulimwengu katika mateso na huzuni.
Wapendwa wengi wamepotea, na janga linaendelea kusababisha mawimbi mapya ya ugonjwa na vifo.
Umasikini, pengo la usawa na njaa vinaongezeka. Ajira zinatoweka na madeni yanaongezeka. Watoto wanahaha.
Ukatili majumbani unaongezeka, na ukosefu wa usalama uko kila mahali.
Lakini mwaka mpya uko mbele yetu. Na tunaona mwanga wa matumaini:
• Watu wanatoa msaada kwa majirani na wageni,
• Wahudumu walio mstari wa mbele wanafanya kila wawezalo
• Wanasayansi wanatengeneza chanjo kwa kasi iliyovunja rekodi
• Nchi zinatoa ahadi mpya ya kuzuia janga la mabadiliko ya tabianchi.
Ikiwa tutafanya kazi pamoja kwa umoja na mshikamano mwangaza huu wa matumaini unaweza kufika duniani kote.
Hilo ndilo fundisho la mwaka huu mgumu zaidi.
Mabadiliko ya tabianchi na janga la COVID-19 ni majanga ambayo yanaweza kushughulikiwa tu na kila mtu kwa pamoja kama sehemu ya mpito kuelekea mustakabali jumuishi na endelevu.
Matamanio makubwa ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2021ni kujenga ushirikiano wa kimataifa wa kuweka mizania ya hewa ya ukaa inayozalishwa na ile inayoondolewa na hatimaye kutozalisha kabisa hewa hiyo ifikapo mwaka 2050.
Kila serikali, jiji, biashara na watu binafsi wanaweza kushiriki ili kutimiza lengo hili.
Pamoja hebu tuweke amani miongoni mwetu na mazingira, tukabili janga la mabadiliko ya tabianchi, tukomeshe kusambaa kwa COVID-19 na tuufanye mwaka 2021 kuwa mwaka wa uponjaji.
Uponyaji kutokana na athari za virusi hatari, kuponya uchumi na jamii zilizosambaratika. Uponyanji wa migawanyiko na kuanza kuiponya sayari.
Hilo ni lazima liwe azimio letu la mwaka mpya 2021.
Nawatakia nyote heri na amani ya mwaka mpya, kutoka Umoja wa Mataifa.
Recent Video On Demand