Available languages:
Katibu Mkuu Wa Umoja Wa Mataifa Ujumbe Wa Video Kwa Siku Ya Kimataifa Ya Kumbukizi Ya Mauaji Ya Halaiki Ya Wayahudi
26 Jan 2021 -  Leo tunakumbuka wayahudi milioni sita na wengineo waliouawa kimfumo na manazi na washirika wao.

Kumbukizi ya mwaka huu inafanyika chini ya kivuli cha janga la COVID-19 ambalo limedhihirisha ufa wa muda mrefu wa ukosefu wa haki na usawa katika jamii na kuchangia kuibuka tena kwa chuki dhidi ya Wayahudi na chuki dhidi ya wageni.

Mauaji ya maangamizi makuu ya Holocust ilikuwa ni kilele cha milenia mbili za ubaguzi, mashambulizi, kufukuzwa na mauaji ya Wayahudi mara kwa mara.

Yanapaswa kuwa yamekomesha uhasama moja kwa moja lakini hayakufanya hivyo.

Kwa bahati mbaya chuki dhidi ya Wayahudi bado iko hai na bado inaendelea.

Ni lazima tufanye juhudi za pamoja haraka kukomesha hali hii.

Leo hii kunaibuka watu wanaodhani weupe ni bora kuliko wengine na wanaounga mkono unazi mamboleo, wakishawishi watu na kuwaingiza katika imani hiyo kila kona ya dunia na kuongeza juhudi zao za kuikana historia, kupotosha na kuiandika tofauti historia hiyo ikiwemo ya mauaji ya maangamizi makuu ya Holocust.

Janga la COVID-19 limewapatia fursa mpya za kuwalenga walio wachache kwa misingi ya dini, rangi, kabila, utaifa, jinsia, ulemavu na hadhi za uhamiaji.

Tuchukue hatua za dharura za pamoja kukomesha vitendo vyao.

Tunapofikiria kujikwamua kutoka katika janga la COVID-19 ni lazima kushughulikia utete na mapengo yaliyofichuliwa na janga hili, lakini pia kuimarisha ushirikiano kwa misingi ya utu wetu.

Mwaka huu lazima uwe mwaka wa uponyaji. Uponyaji kutoka janga la corona na uponyaji wa jamii zetu zilizoparaganyika, ambamo kwazo chuki imeota mizizi. Tunapowakumbuka waliokufa kwenye Holocust na kuwaenzi manusura zawadi yetu bora itakuwa ni kuunda dunia yenye usawa, haki na utu kwa wote.
Open Video Category